Sunday, Feb 18th

Tume ya Haki za Binadamu, UNESCO Wataka Jamii Kutambua Haki za Watu Wenye Ualbino Nchini

  • PDF

Kamishna wa CHRGG Dr. Kevin Lothal Mandopi akiongea na waandishi wa habari na wadau wengine wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelimishaji umma kuhusu ualbinoTume ya Haki za binadamu na Utawala bora  nchini,  leo Juni 13,2015, imeungana na watanzania wote kuadhimisha siku ya Kimataifa ya uelimishaji umma kuhusu ualbino na haki za watu wenye ualbino ambapo imeitaka jamii kutambua haki na wajibu wa kuwalinda na kuwathamini.

Akisoma taarifa maalum kwa wadau mblimbali  na waandishi wa habari waliojitokeza jijini Dar Es Salaam, Kamishna wa tume hiyo, Dkt. Kevin Lothal Mandopi alieleza kuwa jamii inayo wajibu wa kuwathamini watu  hao wenye albinism  kwani nao ni kama  binadamu wengine na wana haki sawa.

Kamishna Mandopi katika taarifa hiyo alibainisha kuwa, mpango wa elimu kwa umma umelenga kubadilisha fikra, mtazamo na imani potofu juu ya watu wenye ualibinism.

“Ni dhahiri kuwa iwapo jamii itaelewa dhana nzima ya ualbinism na kubadili fikra na dhana potofu dhidi ya watu hawa, kuna uwezekano mkubwa wa kukomesha kabisa matendo maovu dhidi ya ndugu zetu wenye ualbinism” alieleza Kamishna Mandopi.

Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Zulmira Rodrigues alisisitiza jamii nchini kuongeza upendo pamoja na kuachana na imani potofu zinazosababisha kukithiri kwa vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino hapa nchini.

Pia alibainisha umuhimu wa kutoa elimu kwa umma juu ya ualibinism ili watu wenye ualbino waishi na kupata haki sawa kama binadamu wengine.

“Wajibu wetu ni kuwathamini na kuwalinda watu wenye ualbinism, nimefika sehemu mbalimbali hapa Tanzania ikiwa ni pamoja na mikoa ya kanda ya ziwa, pia nimetembelea vituo maalum vya watoto wenye albinism. Ni wakati wa kuendelea kutoa elimu ili watoto hao watoke huko ili waishi na jamaa zao kama watu wengine” alisisitiza Bi. Zulmira.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Marry Massay alizitaka mamlaka husika ikiwemo za serikali na watu binafsi, vyombo vya habari na jamii kwa pamoja kutoa elimu ya uelimishaji umma kuhusiana na ualbinism ili kuendelea kuijenga Tanzania yenye amani na upendo kama ilivyojizolea sifa ndani na nje ya mipaka yake.Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO Bi. Zulmira Rodrigues akiongea wakati wa mmadhimisho hayo

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bi. Neema Ringo, alibainisha kuwa, ofisi yake imekuwa mstari wa mbele kufuatilia kesi mbalimbali zikiwemo kesi dhidi ya unyanyasaji kwa jamii ya watu wenye albinism huku akiwataka wananchi kujitokeza kutoa ushahidi pamoja na kufuatilia kesi hizo mara kwa mara.

Kwa upande wao, wadau waliohudhuria waliitaka serikali kuwa mstari wa mbele kushikamana na jamii hiyo yenye ualbinism ili kutokomeza kabisa imani potofu iliyojijengeka kwa watu, ikiwemo kutoa elimu kwa ngazi zote mara kwa mara.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kimataifa ya kuongeza ufahamu juu ya ualbino ambayo yameandaliwa na Chama Cha Albino Tanzania, jijini Arusha.